About the Journal

Jarida la Bahari ya Lugha:Kiswahili na Taaluma zake (JBL) ni Jarida la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar lenye namba ya usajili ISSN: 3142-5658, eISSN: 3142-5704. Jarida hili linaweza kukufikia kwa urahisi mtandaoni na pia kupitia kwenye nakala ngumu ya jarida iliyochapishwa. JBL ni jarida la lugha ya Kiswahili na taaluma zake zikiwemo Lughawiya, Fasihi, Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kiswahili kama Lugha ya Pili, Kiswahili na Teknolojia, Tafsiri na Ukalimani, Kiswahili na masuala mtambuka na nyengine  zinazohusiana na Kiswahili. Jarida hili linachapisha makala mara mbili kwa mwaka (Toleo la Juni na Disemba). Toleo maalum linaweza kuandaliwa na kuchapishwa wakati wowote, bila kuathiri matoleo mawili ya kawaida ya jarida.

Lengo la jarida ni kusambaza matokeo ya tafiti mbalimbali zinazohusiana na lugha ya Kiswahili duniani kote. Pia kuchochea uzalishaji, usambazaji na matumizi ya maarifa mapya katika taaluma za lugha na nyanja nyengine zinazohusiana nazo. Jarida la Bahari ya Lugha ni la kitaaluma, linapitiwa kwa kutumia kanuni ya wahakiki wasiowekwa bayana (double-blind peer review).  

Jarida linapokea makala za awali ambazo hazijawahi kuchapishwa wala kuwasilishwa kwa wakati mmoja katika jarida jengine. Uwasilishaji wa awali wa mswada hadi uamuzi wa mwisho wa uchapishaji makala, pamoja na taarifa zote za mawasiliano yatafanyika ndani ya mfumo. Kila mswada utapelekwa kwa angalau wapitiaji wawili wenye uzoefu na utaalamu katika eneo husika la mswada.

Kila makala itakaguliwa na mhariri ili kuona kama inalingana na malengo na upeo wa jarida pamoja na kuangalia kigezo cha kuhushi (plagiarism). Mswada utakaoonekana unafaa kwa mtazamo wa awali utatumwa kwa wataalamu wasiowekwa bayana kwa ajili ya mapitio na kushauri ama kukubaliwa au kukataliwa kuchapishwa. Ikiwa mswada utakosa vigezo vya msingi, mhariri anaweza kuukataa moja kwa moja (desk reject) mswada huo.